HabariLifestyleNews

Viongozi wa Mombasa waungana kupinga kuruhusiwa kwa Jumuiya ya LGBTQ

Viongozi wa Vuguvugu la kupinga mapenzi ya jinsia moja kuanti ya Mombasa –ANTI-LGBTQ pamoja na viongozi wa Kidini na kisiasa wameongoza mandamano ya amani kupinga uamuzi wa mahakama ya upeo unaoidhinisha usajili wa mashirika ya jumuiya ya LGBTQ na uwepo wa suala hilo nchini.

Katika maandamano hayo ya siku ya Ijumaa (Septemba 15) mashirika ya kijamii, viongozi wa kidini na viongozi wa kisiasa waliungana kukemea uamuzi huo.

Salim Karama ambaye ni Mwenyekiti wa Vuguvugu la kupinga mapenzi ya jinsia moja kaunti ya Mombasa alisema uamuzi huo utaathiri pakubwa vizazi vijavyo huku akitaja maswala hayo kuwa kinyume na maadili na tamaduni za kiafrika.

“Jambo hili ni liweke wazi sababu tuna hofu hasara kubwa ambayo itatokea katika watoto wetu.Leo kuna NGO’s ambayo wametuletea barua ya kusema kuwa sisi ni Al-shabaab na kusema kuwa sisi ni wauwaji,tuko wazi na tunatoa wito kwa serikali wafanye uchunguzi na kuangalia kama sisi tuko na mawasala ya ugaidi au kuua.” Alikariri Karama.

Aidha alibainisha kuwa kuna baadhi ya mashirika ya kupigania haki za kijamii ambayo yamewatishia kutoendeleza juhudi za kupinga maswala hayo humu nchini na kuliorodhesha vuguvugu hilo kuwa la kigaidi.

 “Hii ni njia ya kutuitia hofu ya kutuonyesha kuwa tunyamazie maswala hao.” Aliongeza.

Kwa upande wake mbunge wa Nyali Mohammed Ali maarufu Jicho Pevu amekemea kuwepo wa suala hilo nchini akidai ni ukiukaji wa katiba ya nchini pamoja na maandiko ya vitabu vitukufu.

Kadhalika alionya mataifa ya ng’ambo dhidi ya kushinikiza itikadi zao kwa mataifa ya bara la Afrika akisema kuwa uamuzi wa mahakama ya upeo unatokana na ushawishi na hofu ya kupoteza ufadhili kutoka mataifa hayo.

“Katiba ya Kenya imekataa kwa hiyo sielewi watu wa mahakama ya upeo walikuwa wanasoma katiba gani. Tutaheshimu uhusiano baina ya Kenya na Marekani lakini hatutakubali kuingiliwa kwa maswala ya nchi hii,we are God-fearing people ,hatutakubali sheria hizo za Marekani.” Alisema Mbunge huyo.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK, Sheikh Mohammed Dor ametoa changamoto kwa wazazi na jamii kwa jumla kuwakuza wanao kwa misingi ya dini ili kuhakikisha kuwa hawajitosi katika lindi hili.

Dor alihimiza ushirikiano wa dini zote katika harakati ya kukabiliana na swala hili.

“Sasa kazi ni kwetu sisi wazazi,ni jukumu letu sisi wazazi,ni jukumu letu sisi viongozi wa dini,ni jukumu letu sisi maimamu wa misikiti kuhakikisha kuwa watoto wetu tumeanza kuwapata kuanzia miaka mitatu ,waweze kujua dini yao,haki na Mwenyezi Mungu.Hapa ni tumefika pahali pabaya sana.” Alisema Sheikh Dor.

Haya yanajiri kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Upeo mnamo siku ya Jumatano, Septemba 12 kuruhusu wapenzi wa jinsia moja LGBTQ kuweza kuunda mashirika na vyama vya kutetea maslahi yao.

BY BEBI SHEMAWIA

Comment here