HabariNews

EACC Yarejeshea Serikai Ekari 32 ya Kisiwa cha Chale.

Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC imerejesha ardhi ya ekari 32 ya kisiwa cha Chale kwa serikali.

Ardhi hiyo ya ekari 32 na yenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 ilikuwa imekunyakuliwa na mabwenyenye.

Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Twalib Mbarak alitangaza kuchukuliwa kwa ardhi hiyo iliyo na sehemu ya msitu wa Kaya na kuorodheshwa kuwa Mbuga ya Bahari na sasa itakuwa chini ya Shirika la Huduma kwa Wanyamapori, KWS.

Akiongea katika kisiwa hicho cha Chale huko Kwale, Mbarak alibaini kujitolea kikamilifu kwa EACC kurejesha ardhi zote zilizonyakuliwa huku akihimiza uongozi wa kaunti hiyo na wananchi kushirikiana kukabiliana na ufisadi.

“Takribani billion 1.2 na kila siku ardhi inapanda bei tunawaomba watu wa KWS na kiwanja hiki kimerudi kwa jamii hivyo tunaomba Gavana uwe macho kwani wezi wa ardho bado wangalipo  na wananchi pia msilale muwe makini kwa kushirikiana na hawa viongozi ili kukabili ufisadi”. Asema Twalib Chale

Kwa upande wake Gavana wa Kwale Fatuma Achani aliitaka tume hiyo kuingilia kati kuchunguza ardhi ambazo wamiliki wake wana hatimiliki bandia kwa kuzifutilia mbali hati miliki hizo.

Akipigia mfano wa shamba la Chenze na Kuranze, Achani alieleza matumaini yake kuwa kwa ushirikiano na tume hiyo ya EACC ardhi hizo na zote zilizonyakuliwa zitarejeshwa kwa serikali.

Kuna wawekezaji wengi bandia ambao wameshika hatimiliki wako ndani ya kaunti hii, hivyo ni naimani tume ya kupambana na ufisadi itashughulika ili watu hao washughulikiwe kikamilifu”,Asisitiza Achani.

Naye seneta wa kaunti hiyo Isa Boi Juma aliwaonya wanyakuzi wa ardhi huku wakitoa hakikisho la kushirikiana na EACC kuchukua mashamba yaliyonyakuliwa.

Mnaona hii ardhi imerudi kwetu sisi, kwa wananchi kwenu na kuichukua kwao tutazidi kuilinda hii ardhi na hakuna mtu ataweza kunyang’anya ardhi hii ya watu wetu hapa Kwale,” alisema Boi.

Haya yanajiri huku tatizo la unyakuzi wa ardhi likionekana kuchukua mkondo mpya kaunti ya Kwale huku visa vya hatimiliki bandia vikitajwa kuchipuka maradufu.

BY BINTI KHAMIS NA MJOMBA RASHID