HabariLifestyleMombasaSiasa

Gavana Achani akemea ukabila, Kwale ikiadhimisha Sikukuu ya Jamhuri

Gavana wa Kwale Fatuma Achani amewasuta vikali baadhi ya Viongozi wa kaunti hiyo kwa kile alichokitaja kuchochea wakazi kikabila kutokana na kubuniwa kwa wasemaji wa baadhi ya jamii akisema kuwa wanalenga kuleta mtafaruku katika kaunti hio.

Akizungumza katika Bustani ya Baraza Park katika maadhimisho ya sherehe za Jamhuri, Achani alikemea vikali muungano huo huku akiapa kusimama kidete kuwafanyia kazi wananchi wa Kwale akisema kuwa baadhi ya viongozi walishindwa kuleta maendeleo kwa wakaazi wa kaunti hiyo wakati walipokuwa mamlakani.

“Nikiingia katika uongozi mashamba yetu yalikuwa yamechukuliwa na tulikuwa na viongozi hapa, gavana Mvurya alikuwa kwa hatamu 2 sikusikia maneno wala fitina wala waduruma kuunda muungano wala wadigo. Wacheni fitina! Na wanafanya hizo fitina wanaona ni Gavana ni mama sasa wanaleta vikundi kujaribu kunitishia, nasema sitishiwi nyau mimi!” Alisema.

Achani aliwataki wakaazi kusimama kidete kukemea hatua hiyo akifichua kuwa tayari serikali yake imekomboa mashamba kadhaa ikiwemo kisiwa cha Chale lengo kuu likiwa kupigana na dhulma za unyakuzi wa ardhi ambazo zimekithiri.

“Tusikubali kuchanganywa na kuvurugwa, tumeishi na akina Maina kama ndugu hapa, leo hii tuikisema Wadigo huku Wakamba wande kule sisi hawa wengine waende wapi? Tunataka kuleta Kaya bombo nyengine hapa, hatutaki Kaya Bombo wala MRC, kama kuna mtu aliibiwa shamba ofisi yangu iko wazi ofisi ya Kamishna wa Kaunti iko wazi na tayari nimeanza kupigani Shamba la Chale, Kisite Mpunguti limerudi nab ado napambana kama Mama gavana na wakili.” Alisisitiza Achani.

Kauli yake ilijiri kufuatia baadhi ya wakazi kumtawaza aliyekuwa balozi Chirau Ali Mwakwere kuwa Msemaji wa jamii ya wadigo jambo ambalo limeleta mhemko wa kisiasa katika baadhi ya viongozi kaunti ya Kwale.

Wakati uo huo Gavana Achani alibaini kuwa kaunti ya Kwale inajivunia matunda ya miaka 10 ya Ugatuzi kutokana na hatua mbalimbali ilizopiga kufaidi mkaazi wa kaunti hiyo.

Achani alisema kuwa Serikali yake imejizatiti kuhakikisha huduma muhimu zinafikia mkaazi ikiwemo uboreshaji wa miundomsingi sawia na kupiga jeki sekta ya elimu.

“Kaunti ya Kwale tunajivunia miaka 10 ya Ugatuzi maendeleo tumeyaona hata tulipo Bustani hii haikuwa hivi jamani, si mnaona? Leo hii ndani ya kaunti hii pia tunajivunia wanafunzi wengi wameza kuenda shule za kitaifa na kulipiwa na serikali,” alisema.

Kwa upande wake kamishna wa Kwale Michael Mwangi aliwahimiza wazazi kuchukua fursa hio kuwahimiza watoto waao kuzingatia elimu aksiema kuwa tayari serikali ya kaunti imejitolea kikamilifu kufanikisha mpango huo.

BY NEWSDESK