HabariNews

Kisunzi cha WanaAzimio! Karua aipinga ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo

Kiongozi wa chama cha Narc Kenya Martha Karua ameikashifu ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (NADCO) ambayo inatarajiwa  kufanyiwa ukaguzi na bunge la kitaifa.

Karua ameyataja mazungumzo hayo kama ya kuwapotezea muda wananchi wa Kenya na kwamba hayakuwa na manufaa wala natija yoyote.

Karua amedai kwamba Serikali ililenga kukatiza mazungumzo hayo tangu mwanzo na kuwa haikuwa na nia yoyote ya kushughulkikia masuala muhimu yaliyowasilishwa na upande wa upinzani ulioongozwa na Kalonzo Musyoka.

Amesema kuwa masuala yaliyoibuliwa na upinzani ikiwa ni pamoja na gharama ya juu ya maisha na heshima ya demokrasia ya vyama vingi nchini bado hayajaafikiwa.

“Angalia suala la ushirikishwaji wa umma katika Ukumbi wa Bomas wakati wa Mazungumzo hayo, yapi na kwa kiasi gani yaliangaziwa hadharani kwenye runinga na yapi tuliyasikia kwa Wananchi na ambayo yamejumuishwa katika ripoti hii? Lawama linashukia Kenya Kwanza, walitupumbaza tu,” alisema Karua.

Kauli yake Karua inazidi kuibua  mkanganyiko na maswali mengi zaidi yasiyo na majibu huku ufa ukionekana kujitokeza katika mrengo wa Upinzani wa Azimio la Umoja.

Hii ni licha ya Kinara wa Azimio Raila Odinga kusisitiza kuwa Upinzani uko imara akipuuzilia mbali kuwepo kwa mgawanyiko wa Viongozi kuhusiana na ripoti hiyo ya Mazungumzo.

Akizungumza kwenye mahojiano na Runinga moja nchini mnamo Desemba 27,  Odinga alidai kuwa maoni tofauti tofauti ya viongozi wenza wa Mrengo huo si mgawanyiko bali ni kile ambacho mrengo huo unahimiza; suala la uhuru wa kujieleza.

Alisema kuwa Azimio iliyoongozwa na Kalonzo Musyoka kwenye mazungumzo hayo ilikuwa imepiga hatua mwafaka katika mazungumzo hasa katika masuala muhimu waliyoyaibua.

“Yale ambayo wanachama wa Azimio wanayazungumzia sasa wanaangazia yale ambayo sisi sote tulikubaliana kuhusu suala la gharama ya maisha,” alisema Raila.

“Kile ambacho watu wahakijui ni kuwa kulikuwa na makubaliano kuhusu masuala muhimu tuliyoyaibua kama Azimio.”

Kulingana na Odinga, suala tata pekee katika ripoti hiyo lilikuwa ni ongezeko la gharama ya maisha, suala ambalo wanachama wa Azimio katika mazungumzo hayo walikariri kuwa lilikuwa mikononi mwa serikali ya Kenya Kwanza.

“Jopo letu lilisema katika ripoti kuwa hawakukubaliana na upande wa Kenya Kwanza kuhusu gharama ya maisha kwa sababu Upande wa Kenya Kwanza ulisema watashughulikia suala hilo (la gharama ya maisha) kwa mtindo wao wenyewe na kwa kasi yao,” alisema Odinga.

Kiongozi huyo wa Upinzani alibaini kuwa mrengo wa Azimio ulichagua kuendelea na mazungumzo ya maridhiano licha ya kukosa kukubaliana kuhusu suala la gharama ya maisha kwa sababu tayari mazungumzo yalikuwa yamepiga hatua na kufanikiwa katika masuala mengine muhimu waliyoyaibua.

BY MJOMBA RASHID