HabariNews

Upinzani ulihujumu Mipango yetu ya Maendeleo Mwaka 2023, adai Rais Ruto

Rais William Ruto alitumia ujumbe wake wa mwaka mpya kuukosoa mrengo wa upinzani nchini akidai umekuwa ukihujumu mipango yake ya maendeleo kwa taifa.

Kwenye ujumbe wake wa Mwaka mpya katikia usiku wa mkesha wa Mwaka Mpya huko Nakuru State Lodge, Ruto alilenga upinzani moja kwa moja kwa madai ya kuvuruga mipango yake ya maendeleo kwa taifa katika mwaka 2023.

Rais aliwashutumu kwa kueneza mgawanyiko, migogoro na machafuko nchini, akiongeza kuwa maombi mengi dhidi ya sera zake yanafadhiliwa na watu wenye maslahi binafsi.

“Mtakubaliana na mimi kwamba kuna jambo la kimsingi lisilo sahihi kwa upinzani bila njia mbadala ambayo dhamira yake ni migawanyiko, migogoro na machafuko. Kuna ubaya katika mashauri yanayofadhiliwa na uhujumu kwa lengo la kuchelewesha, kupotosha kuhujumu uwasilishaji wa programu za umma na kuharibu maslahi ya umma,” alisema.

Kiongozi wa taifa pia alitetea serikali yake akidai baadhi ya mikakati iliyowekwa ya kuongeza ushuru imeanza kuzaa matunda na kufufua Uchumi.

Alisema hadi sasa thamani ya shilingi ya Kenya imeanza kuongezeka kwa asilimia 6.8 huku Uchumi ukikua kwa asilimia 5.4 na kuiweka kenya kwenye ramani ya dunia kama taifa nambari 29 linalokuwa kwa kasi zaidi.

“Tuliamua kupunguza matumizi hadi shilingi bilioni 400 ili kupunguza mtindo wetu wa kuomba mikopo na tukaamua kuimarisha ushuru na mapato yetu kwa shilingi bilioni 600 kufadhili mipango yetu na maendeleo ili kulinda taifa letu na uhuru wake, kwa hakika hatuwezi kuendelea na kuwa huru iwapo tutalemazwa na mizigo mizito ya madeni ya kupindukia.” Alisema

Katika hotuba yake hiyo, Kiongozi wa Taifa alidokeza kuwa serikali imekuwa mbioni Kutekeleza miradi mbali mbali yenye manufaa kwa Mkenya.

BY MJOMBA RASHID