HabariNews

Polisi wachunguza vifo vya watu 2 waliouawa eneo la Mwakirunge, Kisauni

Idara ya Polisi eneobunge la Kisauni Kaunti ya Mombasa imeanzisha uchunguzi baada ya wakazi waliokuwa na ghadhabu kumwua mshukiwa wa wizi huko wadi ya Mwakirunge.

Hii ni baada ya mshukiwa huyo pamoja wa wenzake kudaiwa kumvamia na kumwua mzee mmoja mnamo Jumapili jioni Disemba 31, katika eneo hilo kwa njia tatanishi.

Inaaminika kwamba kundi hilo la washukiwa wa ujambazi ambao hujifanya maafisa wa polisi walimchukua mzee Kashaha Mangale nyumbani kwake na kisha kumpiga kwa vifaa butu hadi kufariki mita kadhaa kutoka nyumbani kwake.

Hali hiyo ilichangia wakaazi kuliandama kundi hilo na kumkamata mshukiwa mmoja na kumwua papo hapo huku wenzake wakifanikiwa kutoroka.

Polisi wamefika eneo hilo na kuichukua miili ya wawili hao na kuipeleka katika hifadhi ya maiti ya hospitali kuu Ukanda wa Pwani maarufu, Makadara.

Wakaazi wa eneo la Mwakirunge wamelalamikia Kuhangaishwa na kundi hilo ambalo huvalia nguo kama za polisi na kisha kuwavamia, kuwaibia, kuwajeruhi na hata kuwaua wakaazi wa eneo hilo.

BY NEWSDESK