HabariNews

MATOKEO YA KCSE MWAKA 2023 KUTANGAZWA ASUBUHI YA LEO.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu anatarajiwa kutangaza matokeo baada ya hapo awali kumfahamisha rais na kumpa nakala ya matokeo hayo.

Duru za habari zinaarifu kuwa Waziri Machogu anatangaza matokeo hayo katika shule ya Wasichana ya Moi mjini Eldoret kaunti ya Uasin Gishu, japo Wizara ya Elimu ingali kutoa tamko na taarifa rasmi kwa vyumba vya habari.

Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Desemba mwaka jana, Waziri Machogu alibaini kuwa watahiniwa 903,260 waliofanya KCSE mwaka huo watajua hatma ya matokeo yao wiki ya pili ya mwezi huu wa Januari.

Matokeo hayo ya KCSE ya 2023 yanasubiriwa kwa hamu ikikumbukwa kuwa mabadiliko ya utoaji alama yatakuwa yanatekelezwa kwa kuzingatia mfumo mpya wa utoaji alama za viwango vya Watahiniwa.

Mtihani wa KCSE wa mwaka 2023 ulikumbwa na wimbi la visa kadhaa vya udanganyifu na majaribio ya wizi wa mtihani.

Kutangazwa kwa matokeo hayo katika shule hiyo ya Moi Girls, kunaandikisha historia ikiwa ni mara ya kwanza kwa Wizara ya Elimu kutoa matokeo ya KCSE nje ya Jumba la Mitihani House jijini Nairobi.

BY EDITORIAL DESK