Mashirika yanaendeleza hamasa Kama njia mojawapo ya kuwaepushia watoto na vijana wa umri mdogo madhara na dhulma za kingono mitandaoni.
Shirika la Child Fund, mojawapo ya mashirika yanayoshughulikia haki na maslahi ya watoto liliandaa warsha ya mafunzo hayo kwa watoto wa shule kutoka kaunti ya Mombasa Agosti 24, 2023.
Warsha hiyo ya siku mbili, ilitoa mafunzo ya utumizi halili wa mitandao kwa wanafunzi na kuwanasihi kukoma kushirikiana au kukubali kufanya mikutano na watu wasiowajua.
Joel Kirimana, Afisa wa Watoto kutoka Shirika la Child Development Worker eneo la Kongowea Gatuzi dogo la Nyali, amesema kuwa ili kushinda vita vya dhulma dhidi ya watoto mitandaoni ni sharti watu walewe mbinu zinazotumika na wahalifu.
“Ili kushinda vita hivi, lazima tujue mbinu wanazotumia wahalifu kwenye mitandao na tuwe macho Zaidi”
Kwa upande wake Mratibu wa Mipango shirika la Child Fund Beatrice Muema, mafunzo hayo yanalenga kutoa hamasa Kwa wanafunzi ili kuwasaidia na kuwakinga dhidi maovu mitandaoni.
“Tumekuja kuhamasisha watoto kupitia mfumo uliopo ndio tuweze kuwafikia na kuwapa ufahamu ya jinsi ya kujikinga na dhulma za mitandaoni na kujua madhara yake ni yapi.”Alisema Muema.
Katika mazungumzo yake, Muema aliwataka Wazazi Kuwa makini na hasa kuwalinda wana wao mitandaoni akisema ni jukumu linalohitaji ushirikiano mkuu.
”Mzazi anajukumu la kumlinda mtoto wake mtandaoni kwa sababu sisi wazazi ndio tunahusika sana tunaweka Wifi kwa nyumba kwa hivyo tunafaa kujua watoto wetu wanafanya nini kule mitandaoni.”Aliongeza Muema
Ikumbukwe kuwa suala la dhulma za kingono kwa watoto mitandaoni limekuwa kero kubwa katika jamii hasa wakati huu ambapo idadi kubwa ya wanafunzi wana uwezo wa kufikia simu za wazazi wao.
Warsha hiyo ilihudhuriwa na wadau kutoka taasisi mbali mbali zikiwemo Idara ya Watoto, Idara ya Polisi Kutoka kitengo cha Uchunguzi kuhusu maswala ya Watoto, walimu, wazazi miongoni mwa wadau wengine.
BY DAVID OTIENO